Kiwango cha COVID -19 chapanda Ujerumani


0

Ikiwa ni siku chache zimepita tangu Ujerumani kulegeza masharti ya amri ya kutotoka nje,kiwango cha maambukizi nchini humo kimeongezeka kwa visa 667 na kufanya idadi iliyopo kufikia 169,218, huku vifo 26 vikiongezeka na kufanya idadi yake kuwa 7,395.

Taarifa zinasema kuwa, kiwango cha makadirio cha maambukizi nchini humo kimepanda hadi zaidi ya 1 kwa siku ya pili kutoka 0.7 iliyokuwepo, kabla Kiongozi wa nchi hiyo, Kansela  Angela Merkel kuwataka viongozi wa baadhi ya majimbo kuruhusu shughuli za kawaida kuendelea, ili kufufua uchumi.

Licha ya ongezeko hilo na tangazo kutoka kwa Kansel Merkel kuruhusu kufungua maduka na wanafunzi kurudi shuleni, maelfu ya watu wameandamana juzi Jumamosi wakitaka vikwazo vyote dhidi ya corona viondolewe.

Zaidi ya watu 3000 wameandamana na polisi wamekubali kuwa baadhi yao wamepuuza kanuni ya umbali kati ya mtu mmoja na mwingine.

Wataalamu wameonya kuwa kiwango cha maambukizi  kitaongezeka kwa kasi  baada ya kuona idadi kubwa ya watu wakitoka nje kuendelea na shuhuli zao.

Ujerumani imekuwa nchi ya sita kwa idadi kubwa ya maambukizi ya virusi vya corona kwa bara la Ulaya. 

 


Like it? Share with your friends!

0