Kenya yaibuka kidedea UN


0

MAREKANI

Kenya imeibuka mshindi katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya ujumbe usio wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia Januari Mosi, 2021, baada ya kuishinda Djibouti katika duru ya pili la uchaguzi uliofanyika New York, Marekani jana.

Ushindi huo umepatikana ikiwa ni siku moja baada ya nchi mbili hizo kushindwa kupata ‘kura za kutosha’ kuchukua nafasi hiyo.

Kenya imeibuka mshindi baada ya kupata kura 129 huku Djibouti ikipata kura 62 kutoka nchi 192 zilizoshiriki, hivyo kuifanya Kenya ifikishe hitaji la theluthi mbili ya kura zote, kwa mujibu wa kanuni za baraza hilo.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ameelezea furaha yake baada ya kufahamishwa kuhusu ushindi huo, akisema kwamba

unaonyesha imani ambayo jumuiya ya kimataifa inayo kwa nchi yake.

Kenya ilitumia mbinu mbalimbali kuzishawishi nchi zingine kuipigia kura. Ilimteua Waziri wa Mambo ya Nje, Tom Amolo kuwa balozi maalum wa kuiongoza kampeni hiyo, akisaidiwa na Balozi Catherine Mwangi na Lazarus Amayo ambaye ni balozi wa Kenya kwenye Umoja wa Mataifa.

Hii ni mara ya pili kwa Kenya kupata nafasi kwenye baraza hilo, iliwahi kuwa mwakilishi wa bara la Afrika kati ya mwaka wa 1996 na 1997.

Baraza la Usalama la UN ni chombo muhimu kwenye mfumo wa Umoja huo kwani lina nguvu za kufanya maamuzi yenye uzito mkubwa kimataifa

Pia lina wanachama watano wa kudumu ambao ni Marekani, China, Russia, Ufaransa na Uingereza, ambazo kila mmoja ana kura ya turufu.

Nchi nyingine 10 huwakilishwa kwa kipindi cha miaka miwili kila moja zikiwemo Niger, Tunisia na Afrika Kusini ambayo awamu yake inafika kikomo mwishoni mwa mwaka huu na nafasi yake sasa itachukuliwa na Kenya.

 


Like it? Share with your friends!

0