Kabendera asomewa kosa la uhujumu uchumi


0

Mwandishi wa habari za uchunguzi, Erick Kabendera (39), aliyekuwa akishikiliwa na Polisi tangu Julai 29 mwaka huu, amefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na kusomewa mashtaka 3, likiwemo la kutakatisha zaidi ya shilingi milioni 173.

Kabendera alipanda kizimbani jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizile na kusomewa mashtaka ya uhujumu uchumi na mawakili wa Serikali watatu ambao ni  Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi, Faraja Nchimbi na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon.

Akisoma shtaka la kwanza, Kadushi, alidai kati ya Januari mwaka 2015 na Julai 2019 maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, Kabendera na wengine ambao hawapo mahakamani, alitoa msaada kwenye genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia fedha.

Nchimbi alisoma shtaka la pili ambalo mshtakiwa anadaiwa kukwepa kodi, kati ya Januari, 2015 na Julai 2019 maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, bila sababu za msingi Kabendera alikwepa kulipa kodi ya shilingi milioni 173,247,047.02 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Wankyo akisoma shtaka la tatu la kutakatisha fedha, alidai kuwa katika tarehe hizo, mshtakiwa alitakatisha kiasi hicho cha fedha huku akijua zimetokana na zao la kusaidia genge la uhalifu na kukwepa kodi.

Hakimu Rwizile alimfahamisha mshtakiwa kwamba Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo, hivyo hakutakiwa kujibu lolote.

Baada ya kumaliza kusikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 75/2019, Mahakama iliendelea kusikiliza maombi yaliyowasilishwa na mawakili wa utetezi.

Wakili Jebra Kambole alidai maombi yaliyopo mahakamani, waliomba mshtakiwa apewa dhamana ama afikishwe mahakamani.

Alidai mshtakiwa amefikishwa mahakamani, lakini kwa mashtaka ambayo hayana dhamana, hivyo kwa upande wao hawana cha kuzungumza, waliomba kuondoa maombi yao na ikaahirishwa hadi Agosti 19, mwaka huu.

 

 

Wakili Kadushi alidai kwa upande wao hawana pingamizi kwa maombi hayo kuondolewa.

Kabendera anatetewa na Wakili Kambole, Reginald Martine, John Mallya, Benedict Ishabakaki na Swedy Shilinde.

Taarifa za kukamatwa kwa Kabendera zilianza kusambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii jioni ya Julai 29, mwaka huu na kuthibitishwa na ndugu zake waliodai kuwa mwanahabari huyo alichukuliwa nyumbani kwake Mbweni, Dar es Salaam na watu waliojitambulisha kuwa ni Polisi.

Siku moja baadaye, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, katika mkutano na waandishi wa habari, alisema Polisi wanamshikilia Kabendera kwa mahojiano kuhusu uraia wake na kwamba alikamatwa baada ya kushindwa kutii wito wa kumtaka kufika Polisi kwa mahojiano.

Hata hivyo siku, moja baadaye Idara ya Uhamiaji ilisema imekuwa ikimfuatilia mwandishi huyo tangu mwaka 2013, baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi ambao wamekuwa wakilalamika kuwa si raia wa Tanzania.

Akitoa ufafanuzi huo, Kamishna wa Uraia na Pasipoti wa idara hiyo, Gerald Kihinga, alisema uchunguzi huo ulianza muda mrefu, lakini yeye alikaidi alipoitwa kutoa maelezo ya upande wake.


Like it? Share with your friends!

0