JPM, asema rushwa ni sababu ya wakandarasi wa Tanzania kunyimwa miradi


-1
-1 points

Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli ametaja baadhi ya sababu zinazofanya wakandarasi wa ndani kushindwa kupewa miradi mikubwa ili kuitekeleza.

Miongoni mwa sababu hizo ni kukosa umoja na ushirikiano kati yao, kuendeleza vitendo vya rushwa, wakandarasi kuwa wazito kuomba zabuni ya kutekeleza miradi mikubwa inayotangazwa nchini na wengine wamekuwa wakishirikiana na wafanyakazi wasio waadilifu wa Serikali kuomba zabuni.

Magufuli amebainisha hayo leo katika mkutano uliowakutanisha watumishi wa bodi tatu zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi ikiwemo, Bodi ya usajili wa Makandarasi (CRB), Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) na Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) jijini Dar es Salaam.

Amesema mwaka jana Serikali ilitangaza mradi wa barabara ya kutoka Chamwino kwenda mjini Dodoma, lakini hakuna kampuni ya Wazalendo iliyoomba tenda hiyo.

“Kuna miradi mingine midogo tu ya kuongeza mita 500 kama ile ya uwanja wa Dodoma, wazalendo hawakuomba, ninaweza nikataja miradi mingi na hapa unaweza ukajiuliza, hawa wazalendo kampuni zao hazijui kuomba kazi, hawana utaalamu wa kufanya au tatizo liko wapi,” amesema

Magufuli amesema wakati mwingine hata miradi ya ndani midogo kabisa ambayo alidhani kampuni za ndani zitaomba hazifanyi hivyo.

 “Lakini wakati mwingine kupata zabuni mmekuwa mkishirikiana na wafanyakazi wasio waadilifu wa Serikali, bado ndani ya Serikali kuna watendaji wasio waadilifu na ndiyo maana wakati mwingine makadirio ya fedha inayowekwa kwenye miradi inakuwa iko juu sana.”


Like it? Share with your friends!

-1
-1 points