Eusebius Nzigilwa Ateuliwa kuwa Askofu wa jimbo la Mpanda


0

Baba Mtakatifu Francisko amemteuwa Askofu Msaidizi Eusebius Nzigilwa kuwa Askofu mpya wa jimbo katoliki la Mpanda mkoani Katavi.

Kabla ya uteuzi huo, Askofu Nzigilwa aliyezaliwa Agosti 14, 1966 jijini Mwanza, alikuwa ni Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Saalam.

Jimbo Katoliki la Mpanda limekuwa wazi kuanzia Desemba 21, mwaka 2018, baada ya Baba Mtakatifu Francisko kuunda Jimbo kuu Jipya la Mbeya na kumteua Askofu Gervas Nyaisonga ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kuwa Askofu Mkuu wake wa kwanza.

Historia fupi ya maisha yake inaonesha kuwa Askofu Nzigilwa alisoma sekondari katika seminari ndogo ya Mtakatifu Petro mkoani Morogoro na mwaka 1988, alishiriki katika mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria, na baadaye alijiunga na Seminari Kuu ya Kibosho mkoani Kilimanjaro.

Alisoma masomo ya falsafa na Taalimungu katika Seminari Kuu ya Kipalapala mkoani Tabora na baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, akapewa daraja takatifu la upadre katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam Juni 23, 1995.

Kati ya 1995 na 1996, Nzigilwa alikuwa ni padre mlezi kwenye nyumba ya malezi iliyopo parokia ya Mtongani Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Aliwahi pia kuwa ni Mkurugenzi wa Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu kuanzia Mwaka 1996 hadi Mwaka 1997. Baadaye Kardinali Polycarp Pengo alimteuwa kuwa Gambera wa seminari ndogo ya Visiga kwa kipindi cha 1997-1999.

Askofu Nzigilwa aliendelea na masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alipotunukiwa shahada ya kwanza ya elimu.

Baada ya masomo yake, aliteuliwa kwa mara nyingine tena na Kardinali Pengo kuwa Gambera wa seminari ndogo ya Visiga kuanzia 2003 hadi 2008, na baadaye Shahada ya Uzamili katika Sayansi ya Elimu chuoni hapo.

Januari 28, 2010, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alimteuwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam na kuwekwa wakfu Machi 19, 2010 wakati wa sherehe ya Mtakatifu Yosefu.


Like it? Share with your friends!

0