Deni la Korosho kumalizwa


0

Serikali imesema itamaliza deni la wakulima wa korosho kabla ya msimu ujao kuanza.

Hayo yameelezwa leo bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Kilimo,  Omary Mgumba wakati akijibu swali la mbunge wa Ndanda (Chadema) Cecil Mwambe, liyetaka kujua ni lini watakamilisha madeni ya wakulima wa korosho kwa kuzingatia Serikali ilisema inazo fedha za kuwalipa.

Katika majibu yake Mgumba amesema kilichotokea ni Bodi ya Mazao Mchanganyiko kuwa imefikia kikomo cha kuchukua fedha katika Benki ya Uwezeshaji nchini (TIB).

Amesema TIB waliwataka kuuza kwanza korosho walizonazo ambazo tayari zimeshauzwa na kwamba kabla ya msimu wa korosho kuanza wakulima hao watakuwa wameshalipwa fedha zao.

Mwaka jana, Serikali, iliingilia kati sakata la bei na kuamua kununua korosho yote iliyopo sokoni moja kwa moja, kwa bei ya juu kidogo tofauti na iliyopangwa na wafanya biashara.

Lakini, miezi mitatu baadae, baadhi ya wakulima bado hawajalipwa huku wengine wakirudishiwa korosho zao kwa madai ya kuwa chini ya kiwango.

Korosho, ambayo miaka yote imekuwa ni dhahabu ya kusini, ni zao ambalo linaongoza nchini Tanzania kuingizia fedha za kigeni.

Hata hivyo, wakulima wa zao hili wamekuwa wakikumbwa na changamoto mara kadhaa.


Like it? Share with your friends!

0