China yatumia dawa ya asili kutibu COVID 19


0

CHINA

China imesema asilimia 92 ya wagonjwa wa corona wa nchi hiyo walitibiwa kwa kutumia dawa ya asili ya kale iliyotengenezwa kwa mitishamba maarufu kama Traditional Chinese Medicine (TCM).

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya nchini humo, dawa hiyo ni maarufu nchini China licha ya kwamba ilizua mjadala kuhusu matumizi yake mtandaoni.

Wataalamu wanasema China inajaribu kuisambaza dawa hiyo ndani na nje ya mipaka yake, lakini wataalamu wa afya bado hawaamini uwezo wake wa kutibu.

Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) limesema wizara ya afya ya China imeweka kitengo maalum cha dawa ya TCM na muongozo wa kukabiliana na virusi vya corona.

Televisheni ya taifa ilidai kuwa dawa hiyo ilifanya kazi katika mlipuko wa miaka ya nyuma ikiwemo kutibu virusi vya Sars mwaka 2003.

Wanaounga mkono dawa ya TCM wanadai kuwa dawa hiyo haina madhara kwa mtumiaji lakini wanasayansi wanasema ni muhimu vipimo vya kisayansi vikafanyika ili kuhakikisha usalama wake.

Taasisi ya afya Marekani ilidai kuwa dawa hiyo inaweza kusaidia kuondoa dalili tu, lakini suala la kutibu corona bado kuna mashaka.

Rais Xi Jiping wa China anasema kuna watu wengi ambao wanapenda dawa hiyo tangu enzi za mababu wa nchini humo.

China imekuwa ikisambaza dawa hiyo na vifaa vyake katika mataifa ya Afrika, Asia na ulaya.

 


Like it? Share with your friends!

0