CHADEMA wataka Polisi ifanye mabadiliko ya mitaala ya mafunzo


0

Chama Kikuu cha Upinzani nchini Tanzania cha Chadema kimemtaka Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro kufanya mabadiliko makubwa ya Jeshi la Polisi kuanzia kwenye mitaala ya mafunzo, sheria na utendaji ili kulifanya kuwa chombo kinachotoa huduma.

Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene imesema hatua hiyo itamfanya IGP Sirro kudhihirisha nia yake ya kutamani kuliacha jeshi hilo likiwa na heshima.

Akieleza matukio ambayo IGP Sirro anapaswa kuyashughulikia, Makene amesema ni pamoja na tukio la kushambuliwa kwa risasi aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu Septemba 7, 2017 akiwa jijini Dodoma.

“Hadi leo Jeshi hilo halijawahi kusema iwapo limemhoji au kumshikilia mtu yeyote kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo la aina yake kuwahi kutokea nchini,” amesema Makene.

Hata hivyo, Serikali imeshasema kwa nyakati tofauti kuwa inamtaka Lissu na dereva wake wafike Polisi kutoa ushirikiano ili kufanikisha kufanyika kwa uchaguzi.

Makene pia ametaja kutoonekana kwa mwandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), Azory Gwanda aliyepotea tangu Novemba 2017, aliyekuwa msaidizi wa mwenyekiti wa chama hicho, Ben Saanane pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibondo mkoani Kigoma, Simon Kanguye.

“Kuanzisha tena uchunguzi wa tukio la kuuawa kwa kupigwa risasi aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Akwilina Akwiline na kuwafikisha mahakamani waliohusika,” amesema.

Ametaja pia tukio la kuteswa na kuuawa kwa aliyekuwa Kiongozi wa Chadema Kata ya Hananasif, John Daniel,  ambaye alikuatwa nyumbani kwake na kisha baadaye akaokotwa akiwa amekufa maeneo ya Coco Beach jijini Dar es Salaam.

“Tumetaja matukio hayo kwa uchache ili kuonyesha  namna ambavyo IGP Sirro anapaswa kujua kuwa tatizo la utendaji wa Jeshi la Polisi nchini, linaangaliwa kwa mwonekano wake wa nje zaidi katika kutimiza wajibu wa kulinda raia na mali zao,” amesema.


Like it? Share with your friends!

0