CCM yajitabiria ushindi uchaguzi Serikali za mitaa


0

Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro kimetamba kujiandaa vyema na kusema kipo tayari kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji  unaotarajiwa kufanyika Novemba 24.

Kimesema kuwa uchaguzi huo ndio kitovu cha kushika hatamu za utawala wa dola, hivyo kitaheshimu sheria na matakwa ya demokrasia na ni kipimo cha kuaminiwa kwa vyama vya siasa kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.

Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro, Shaka Hamdu Shaka, alitoa kauli hiyo wakati akitoa tathmini ya uchukuaji fomu za kuomba kuteuliwa na chama kugombea nafasi ya vitongoji, alipokuwa akizungumza na viongozi wa kata, matawi na mashina mjini hapa.

Shaka aliwataka viongozi hao waendelee kujipanga kwa kufuata kanuni, taratibu za kisheria na kikatiba zilizowekwa na Serikali.

Alisema kila kiongozi wa CCM ana wajibu wa msingi kuhakikisha chama kinapitisha wagombea wenye weledi na sifa, wanaokubalika kwa jamii na watakaokuwa tayari kuwatumikia wananchi.

Shaka alisema wakati uchaguzi huo ukifanyika Novemba, Serikali za CCM zimejitahidi vya kutosha kuimarisha huduma za kiwajibu kwa jamii, kuinua uchumi na kushughulikia kero sugu na kuzitatua.

“Nawapongeza sana makatibu wa wilaya, kata na matawi. Hamasa na mwitikio kwa wana-CCM umekuwa mkubwa katika kuchukua fomu za vitongoji ndani ya chama, tunaendelea kusisitizana kuwa uchaguzi huu ni muhimu kwa mustakabali wa chama.

“Mtendaji yeyote wa chama atakayezembea atahesabiwa ni msaliti na amekihujumu chama, usaliti na hujuma si sifa njema, bali ni dhambi isiyosameheka,” alisema Shaka.

Aidha aliwakumbusha watendaji hao wa chama muda wote kuzingatia maelekezo ya kikanuni na kisheria kuhusu usimamizi na kufuata taratibu, miongozo na kanuni za chama na Serikali ili kutimiza dhana ya demokrasia kivitendo.

“Tunashiriki uchaguzi kwa kujiamini tutashinda kwa haki usawa na amani. CCM Mkoa wa Morogoro tunaahidi kufuata taratibu zote za kikanuni na kikatiba, tutakaposhindwa tutaheshimu matokeo na wenzetu pia wawe waungwana wa kutii matakwa na uamuzi wa wananchi,” alisema Shaka.


Like it? Share with your friends!

0