CCM yaendeleza vita kwa wanachama wake


0

Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula, ameonya wanachama wa chama hicho wanaojipenyeza kuwania ubunge na udiwani wakati viti hivyo bado vina watu.

Alitoa onyo hilo Wilaya ya Ikungi mkoani Singida wakati wa mkutano wa kuwapongeza wanaCCM wa Jimbo la Singida Mashariki, baada ya Miraji Mtaturu kutangazwa kuwa mbunge akimrithi Tundu Lissu.

“Natoa maelekezo kuwa mtu yeyote atakayebainika kuanza kujipenyeza kwenye majimbo kuanza kufanya kampeni ya kuwania nafasi hizo za uongozi hatutamwonea huruma, tunamchukulia hatua za kinidhamu,” alisema Mangula.

Alisema katika majimbo kuna wawakilishi ambao muda wao wa miaka mitano bado haujaisha, hivyo waachwe watekeleze ilani ya chama hicho kwa kuwapelekea wananchi maendeleo.

Ametoa maagizo kwa wanaCCM kuwa pindi watakapomwona mtu yeyote ameanza kujipenyeza katika majimbo hayo, watoe taarifa ili aweze kuchukuliwa hatua kupitia kamati ya maadili.

Mangula ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya chama hicho, alielezea umuhimu wa kutoa elimu ya mpigakura ili kila mtu aweze kujua haki yake ya kupiga kura.

Alisema katika uchaguzi mkuu uliopita katika baadhi ya maeneo, watu waliojitokeza kupiga kura walikuwa wachache kutokana na kutokuwepo kwa elimu hiyo.

Mangula ameongeza kuwa hali hiyo ilifanya kiongozi achaguliwe kwa kura chache, akitolea mfano Jimbo la Igalula mkoani Tabora ambako idadi ya wapigakura walikuwa ni asilimia 22 pekee.


Like it? Share with your friends!

0