Boti yawaka moto Ziwa Victoria


0

Watu 56 wamenusurika kifo baada ya boti waliyokuwa wakisafiria katika ziwa Victoria mkoani Kagera kuwaka moto.

Boti hiyo ilikuwa ikitoka Wilaya ya Bukoba kwenda Rushonga wilayani Muleba.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Revocatus Malimi amesema boti hiyo iliyokuwa na abiria 56 pamoja na mizigo, ilianza safari jana mchana Jumatatu Septemba 16, 2019 lakini baada ya muda mfupi ilishika moto, kugeuzwa kurejea bandarini.

Amesema abiria wote waliokuwa katika boti hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 84 waliokolewa na watu waliokuwa ufukweni, baadhi waliweza kuogelea wenyewe.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco  Gaguti amewapa pole wananchi hao, kuwataka kuhakikisha wanazingatia usalama wao wakati wa kusafiri sambamba na wakaguzi wa vyombo vya majini kufanya ukaguzi.

Gaguti na kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa huo umewatembelea majeruhi watatu wa ajali hiyo ambao ni,  Elizabeth Msiwa (28), Agnes Wiliam (42) na Mariam Deus (30).


Like it? Share with your friends!

0