Barrick yaweka wazi nia ya kuinunua Acacia


0

Kutokana na mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka miwili baina ya Serikali na Acacia, Kampuni ya Barrick Gold Corporation imetoa ombi la kununua hisa zote za Acacia, ili kuwa na sauti moja kwenye mazungumzo yanayoendelea.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Makamu wa Rais wa Uhusiano wa Umma wa Barrick, Deni Nocoski amesema kampuni hiyo imekutana na menejimenti ya Acacia na kuwasilisha pendekezo la kununua asilimia 35 ya hisa ambazo haizimiliki.

 “Barrick imekuwa na majadiliano na Serikali ya Tanzania kwa miaka miwili iliyopita kutafuta suluhu ya kudumu kwenye mgogoro wake na Acacia, ili uzalishaji uendelee kama kawaida na kurudisha uhusiano uliokuwepo zamani. Hata hivyo Serikali haikuwa tayari kuzungumza chochote na Acacia”

Taarifa hiyo pia imeeleza ili kufanikisha ununuzi wa Acacia inayokadiriwa kuwa na thamani ya Dola milioni 787, Barrick imependekeza kubadilisha hisa zake na wamiliki wachache wanaobaki Acacia.

Katika thamani hiyo, tathimini inaonyesha kuwa asilimia 35 ya wanahisa wanaobaki Acacia wanamiliki Dola milioni 285, hivyo endapo ombi hilo litakubaliwa, wanahisa waliobaki watakuwa sehemu ya wanahisa wa Barrick, na kwa dhana hiyo mazungumzo yaliyopo kati ya Serikali na kanuni hiyo yataendelea kama kawaida na kutekelezwa kwa wakati.

Hata hivyo Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi, amesema kuwa msimamo wa Serikali uliopo ni kuiondoa kabisa Acacia, isihusike kwa namna yeyote kwenye migodi inayomilikiwa na Barrick hapa nchini.

Dk Abbasi ameongeza kuwa Barrick ndiye mwanahisa mkubwa, na Serikali haitambui Acacia kwa sababu kampuni hiyo tanzu kwa kipindi ambacho ilikuwa inasimamia shughuli za Barrick, ilikiuka sheria na utaratibu mwingi.


Like it? Share with your friends!

0