Afrika wamlilia Nkurunziza


0

BURUNDI

Viongozi mbalimbali barani Afrika wametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza.

Serikali ya Burundi ilitangaza siku ya jana Jumanne kuwa, Nkurunziza amefariki kutokana na mshtuko wa moyo ikiwa ni siku chache tangu mke wake, Denise Bucumi Nkurunziza kulazwa hospitalini jijini Nairobi, Kenya kutokana na kuugua COVID – 19.

Rais John Magufuli ameelezea kushtushwa kwake na taarifa za kifo cha Nkurunziza, na kwamba atamkumbuka kwa uongozi wake imara na juhudi za kupigania amani, maendeleo na kuruhusu demokrasia nchini mwake.

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed ameandika kwenye ukurasa wake wa twitter akielezea kutuma salamu zake za pole kwa raia wa Burundi kufuatia kifo cha gafla cha Nkurunziza

 

Naye Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ametoa pole kwa wananchi wa Burundi na kusema, Nkurunziza alifanya kazi kwa bidiii bila kuchoka; na kwa amani na utulivu kwa ajili ya nchi yake na ukanda wa maziwa makuu.

Viongozi wengine waliotuma salamu zao za rambirambi ni pamoja na Rais wa zaman wa Nigeria Goodluck Jonathan na Mohamed Abdullahi Mohamed wa Somalia.

 

Kwa mujibu wa mtandao wa EastAfrican, wakati Nkurunziza akiaga dunia kutokana na mshituko wa moyo jijini Bujumbura, mke wake Denise bado yupo nchini Kenya akiendelea kupata matibabu.

Nkurunziza alitarajiwa kukabidhi madaraka August mwaka huu kwa Rais mteule, Evariste Ndayishimiye aliyeshinda Uchaguzi Mkuu wa Mei mwaka huu.

Kwa mujibu wa shirika la utangazaji la Ujerumani (DW), Katiba ya Burundi inaelezea utaratibu wa utawala kinapotokea kifo cha Rais, kwamba Spika wa Bunge ndiye anayekaimu nafasi hiyo.

 

Pascal Nyabenda ndiye anayepaswa kushika hatamu za uongozi kwa kipindi cha miezi miwili hadi atakapoapishwa Evariste Ndayishimiye aliyeibuka na ushindi kwenye uchaguzi wa rais wa Mei 20 mwaka huu.

Hata hivyo, hatua hiyo inaweza kuzua utata kutokana na Spika aliyekuwepo, Pascal Nyabenda, kuliongoza Bunge lililovunjwa Aprili 27, mwaka huu ili kuruhusu kampeni za Uchaguzi Mkuu.

Pumzika kwa amani Pierre Nkurunziza.

 

 


Like it? Share with your friends!

0