13 ndani ya CCM wajitokeza kumrithi Lissu


0

Wanachama 13 wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania wamejitosa kupitishwa na chama hicho kugombea ubunge wa Singida Mashariki lililokuwa likiongozwa na Tundu Lissu wa Chadema.

Miongoni mwa waliochukua fomu kuwania nafasi hiyo ni Mkuu wa wilaya (DC) ya Ikungi mkoani Singida, Miraji Mtaturu na aliyewakuwa mkuu mkoa wa Songwe (RC) Chiku Galawa.

Wengine waliochukua fomu juzi na kuzirejesha jana Jumatano saa 10 jioni ni Jeremia Ihonde, Lazaro Msaru, Hamisi Maulidi, Mariamu Nkumbi, Martini Lissu, Slevester Meda, Thomas Kitima, Emmanuel Hume, Mwanahamisi Mujori, Moris Mukhoty na Silinde Kasure.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya shughuli ya urejeshaji fomu kumalizika, Katibu wa CCM wilaya ya Ikungi, Noverty Kibaji alisema wagombea hao watachuana kwenye mkutano wa kura za maoni.

Alisema baada ya hapo watakaoshinda nafasi tatu za juu majina yao yatapelekwa kwenye vikao vya juu vya chama na mwisho wa siku atapatikana mshindi atakayepeperushwa bendera ya CCM kuwania ubunge.

Kibaji aliwaasa wagombea hao wawe wamoja na wapendane kuanzia sasa hata baada ya mshindi kupatikana na kuwaonya kutoanzisha kampeni kabla ya muda uliowekwa

Uchaguzi huo utakaofanyika Julai 31, 2019 unatokana na Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai kusema Lissu kapoteza sifa za kuwa mbunge kutokana na kushindwa kutoa taarifa kwake ya wapi alipo lakini kutokujaza fomu za mali na madeni za maadili kwa viongozi wa umma.

Kutokana na hatua hiyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Ijumaa Julai 05, 2019 Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage alitangaza ratiba ya uchaguzi mdogo wa ubunge huo utafanyika Julai 31 mwaka 2019.

Jaji Kaijage alisema uteuzi wa wagombea utafanyika Julai 18 mwaka 2019 na kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia Julai 19 hadi 30 Julai 2019 na siku ya uchaguzi itakuwa Julai 31, 2019.


Like it? Share with your friends!

0